Tuesday, September 3, 2013

URAIA GRADE 1A AGGREY TEACHER'S COLLEGE



Uraia grade a
Nukuu za somo
Katiba
Uchaguzi wa kidemokrasia









Na. Ntumbitumbi mn


KATIBA YA NCHI
Maana – Ni Jumla ya mambo yote/mwongozo unaotumika kuiongoza nchi katika nyanja zote za kiuchumi, kiutamaduni na kijamii ili kuleta usawa miongoni mwa raia wa nchi husika.
Serikali inachukua madaraka na mamlaka ya kuongoza wananchi katika nchi husika kwa kufuata na kutumia katiba hiyo. Hivyo basi katiba ni sheria mama ambapo sheria zote na miongozo hutolewa humo.
Taarrifa Zinazopatika Katika Katiba
Katika katiba Taarifa za msingi zifuatazo zinapatikana:-
a.       Kichwa, kazi na mamlaka ya mkuu wa nchi.
b.      Madaraka ya bunge na namna wanavyochaguliwa.
c.       Madaraka ya serikali na baraza la mawaziri
d.      Madaraka/mamlaka ya Mahakama na kazi zake.
e.       Kueleza haki na wajibu wa raia
Mambo mengine yaliyopo katika Katiba ya kidemokrasia katika nchi kama Tanzania ni:-
a.       Haki ya kuishi
b.      Haki ya kumiliki
c.       Uhuru wa kushirikishwa na kushiriki katika maamuzi
d.      Uhuru wa kujumuika na kujieleza miongoni mwa watu
e.       Uhuru wa kuabududu
Aina za katiba
Katiba imegawanyika katika makundi makuu mawili, nayo ni:-
a.       Katiba ya kuandikwa
b.      Katiba isiyoandikwa
A.  Katiba ya Kuandikwa
Ni katiba ambayo taratibu, kanuni na mipango ya kisheria imehifadhiwa katika maandishi. Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazotumia katiba iliyoandikwa. Katiba ya kuandikwa ina faida na hasara kama zifuatazo:-
Faida za katiba iliyoandikwa
           i.            Ni rahisi kutumia, kutekelezeka na uhakika.
         ii.            Inasomeka na kufafanua dhana zote za msingi
       iii.            Inaeleza mamlaka na mahusiano kati ya mihimili mingine ya dola
       iv.            Inaeleza kwa uwazi haki na wajibu wa raia na kulinda Uhuru wa mtu mmoja mmoja.
Hasara za katiba iliyoandikwa
        i.      Baadhi ya katiba zilizoandikwa zimeandikwa kwa ujumla sana. Hivyo inasababisha kutoeleweka kwa uraisi
      ii.      Haiwezi kupokea mabadiliko ya haraka. Hivyo haiendani na wakati.
    iii.      Machakato wa kubadili huwa wa taratibu sana, hivyo unafanya mambo kuwa mengi na upotevu wa muda.
    iv.     Inatumia gharama kubwa katika Maandalizi yake
      v.     Inaongeza ubaguzi kwa kutoa manufaa kwa Wasomi pekee na wanaojua kusoma
B.  Katiba Isiyoandikwa
Ni katiba ambayo haijaandikwa katika nyaraka moja. Uingereza ni mfamo wa nchi inayotumia aina hii ya katiba katika maamuzi yake nchini.
Tabia za katiba Isiyoandikwa
Katiba isiyoandikwa huwa na tabia zifuatazo:-
a.       Inaweza kupokea mabadiliko kwa haraka
b.      Inaweza kutumika katika mataifa makubwa zaidi
c.       Sio nzuri kwa mataifa machanga
d.      Pia ni rahisi kuboresha kwa maslahi ya wananchi

Faida za Katiba Isiyoandikwa
        i.            Haina gharama kubwa
      ii.            Hubadilika kwa haraka kulingana na mahitaji ya watu
    iii.            Mabadiliko yake uchukuwa muda mfupi sana
Hasara za Katiba Isiyoandikwa
        i.            Sio nzuri kwa mataifa machanga kama Tanzania
      ii.            Inahitaji serikali imara sana
    iii.            Inatumia nguvu kama watawala wasipokuwa makini.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ni katiba iliyoandikwa katika kwa kuzingatia mambo ya msingi yafuatayo:-
a.       Misingi ya Demokrasia
b.      Haki za Binadamu na Uhuru
c.       Maamuzi ya kidplomasia
d.      Kuangalia Uhuru wa nchi na mataifa mengine
A.  Misingi ya Kidemokrasia
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaagiza na kushauri kuwa raia wa nchi hii ndio watakazo tengeneza/kuunda serikali yao. Serikali inapata mamlaka na nguvu za kutawala kutoka kwa wananchi.
B.  Haki za Binadamu na Uhuru
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya Azimio la haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa, Katiba imetaja haki mbalimbali za binadamu. Haki hizo ni kama zifuatazo:-
          i.            Haki ya kuzungumza
        ii.            Haki ya kushirikishwa na kushiriki
      iii.            Haki ya kuwa na maisha mazuri
      iv.            Haki ya kumiliki mali
        v.            Haki ya kuabudu
      vi.            Haki ya kuoa au kuolewa na kuunda familia
    vii.            Haki ya kuishi
C.  Misingi ya Maamuzi ya Kidiplomasia
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema kuwa lazima kuwe na usalama na usawa kwa raia wote kabla ya sheria. Hivyo hakuna raia wa nchi hii ambaye yupo juu ya sheria.
D.  Kuangalia na Kulinda Uhuru wa Nchi na Mataifa Mengine
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasema nchi ya Tanzania lazima iwe huru na nchi nyingine zinazopakana na Tanzania. Hivyo katiba ya Tanzania inaeleza Uhuru wa umoja. Hivyo katiba ya Tanzania inaeleza na kusisitiza na Kuangalia amani katika mataifa mengine pia. Hiyo inatokana na kuhakikisha maamuzi ya ndani hayaingiliwi.
Sura za Katiba
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imegawanyika katika sura tisa baada ya mabadiliko ya 1977-2005.
Sura ya Kwanza ya Katiba
Katika sura ya kwanza, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza Jamhuri ya Muungano kuwa ni nchi yenye serikali ya kidemokrasia inayoundwa na kutumia muundo/mfumo wa vyama vingi. Ni nchi ya kijamaa kwa asili.
Pia katika sura hiyo katiba inaeleza kuwa Tanzania nchi ya Muungano. Hivyo ni Muungano wa nchi wa mbili ambazo ni Tanganyika na Zanzibar, hapo ndipo ilipozaliwa Jamhuri Muungano wa Tanzania. Tanzania ina serikali mbili, serikali ya Muungano na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, na serikali hizo zina marais, bunge na Mahakama. Sehemu ya tatu ya sura ya kwanza ianeleza haki na wajibu wa watu, haki zinazo taja hapa ni kama usawa, haki ya kuishi, haki ya kuwa huru, kusikilizwa na kufanya kazi.
Sura ya Pili ya Katiba
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Sehemu ndogo ya kwanza inaeleza madaraka na nguvu ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
          i.            Mkuu wa nchi
        ii.            Kiongozi mkuu wa serikali
      iii.            Amiri jeshi mkuu wa majeshi
      iv.            Muwakilishi katika Umoja wa Mataifa/Nje ya nchi
Sehemu ndogo ya pili inaeleza kuhusu makamu wa rais wa Tanzania, na kueleza mamlaka na wajibu wake. Sehemu ndogo ya tatu inaeleza haki, wajibu wa bunge
Sura ya Nne ya Katiba
Sura ya nne ya katiba ya Jamhuri ya Muungano inahusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baraza la wawakilishi.
Sura ya Tano ya Katiba
Sura ya tano sehemu ya kwanza inaeleza Mahakama kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sehemu ya pili inaeleza Mahakama kuu ya Zanzibar. Sehemu ya tatu inaeleza Mahakama ya rufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sura ya Sita ya Katiba
Sura ya sita inaeleza tume ya malalamiko na maadili ya viongozi
Sura ya Saba ya Katiba
Sura ya saba inaeleza masuala ya fedha katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sura ya nane na tisa inafanya majumuisho ya mambo yote katika katiba.
Mabadiliko ya Katiba Tanzania
Katiba ya kwanza ya Tanganyika iliandikwa mwaka 1961 chini ya usimamizi wa waingereza. Malkia wa Uingereza alikuwa anaendelea kuwa mkuu wa taifa jipya. Kwa Tanganyika Malkia alikuwa anawakilishwa na Gavana Mkuu ambaye alikuwa anaitwa Sir. Richard Turnbull. Wakati huo waziri mkuu alikuwa Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa mkuu wa serikali. Lakini wakati huo Malkia alikuwa na mamlaka ya kuvunja bunge na kuitisha uchaguzi. Mkuu wa majeshi ya ulinzi alikuwa mwakilishi wa Malkia.
Katiba ya pili ilibadilika mwaka 1962, Desemba 9. Katiba hiyo ndiyo iliyounda Tanganyika kuwa Jamhuri. Katiba hiyo ilitoa nguvu na mamlaka kwa Tanganyika kuwa na maamuzi nje ya nchi na ndani ya nchi. Rais akawa ndiyo mkuu wa nchi na serikali.
Katiba ya kwanza ya Zanzibar iliundwa mwaka 1963 Desemba, 10. Lakini katiba hiyo haikuwasaidia Zanzibar kuwa taifa lenye Uhuru. Wakati huo Sultani wa Kiarabu alikuwa ndiye mkuu wa nchi wakati waziri mkuu alikuwa Kiongozi mkuu wa serikali.
Tarehe 12 Januari, 1964, Sultani alipinduliwa na Wazanzibar. Sheikh Aman Karume akawa ndiye rais wa kwanza wa Zanzibar akawa pia ndiye mkuu wa nchi na serikali. Tanganyika na Zanzibar wakaunda Muungano wa serikali 26, April 1964. Muungano huo uliunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuandaa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano.
Katiba ya Mpito
Baada ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katiba mpya iliundwa mwaka 1965 mwezi januari. Katiba ilieleza rais akitoka Tanzania bara, makamu wa rais atatoka Zanzibar. Makamu wa pili wa rais atatoka Tanzania bara. Mwalimu J. K. Nyerere akawa rais na Sheikh Abeid Amani Karume alikuwa makamu wa kwanza wa rais, bwana Rashidi Mfaume Kawawa alikuwa makamu wa pili wa raisi. Mwaka 1965 Tanzania ilikuwa nchi ya chama kimoja. ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanzania bara.
Katiba ya Mpito, iliunda serikali mbili, serikali ya Muungano na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar. Mwaka1977 Katiba ya Kudumu iliundwa. Hii ndio katiba inayotumika hadi sasa. Lakini mabadiliko/marebisho ya katiba yalifanyika katika katiba hiyo. Mwaka 1984 rais alipunguziwa muda wa kuwa madarakani hadi vipindi viwili vya miaka miaka mitano. Mwaka 1992, Julai mfumo wa vyama vingi uliundwa Tanzania. Mwaka 1994, rais wa Zanzibar alikoma kuwa makamu wa rais katika serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Marekebisho ya Katiba
Bunge la Jamhuri ya Muungano ndiye taasisi au chombo pekee ambayo kinaweza kufanya mabadiliko ya Katiba. Marekebisho ya Katiba ufanyika kwa kupiga kura. Mambo yafuatayo yanaweza kufanya marekebisho ya Katiba, kama 2/3ya wabunge kutoka baraza la wawakilishi Zanzibar na 2/3 ya wabunge kutoka Tanzania bara kupiga kura ndiyo:-
            i.            Uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
          ii.            Uwepo wa ofisi ya Rais
        iii.            Madaraka ya serikali ya Muungano
        iv.            Uwepo wa bunge la Muungano
          v.            Mamlaka ya serikali za Tanzania na Zanzibar
        vi.            Mambo ya Muungano
      vii.            Idadi ya wabunge kutoka Zanzibar
Mambo yaliyobaki yanaweza kufanyiwa marekebisho kama 2/3 ya Jumla ya wabunge wakiunga mkono.
Maswali
1.      Katiba ni nini?
2.      Katiba imegawanyika katika makundi yafuatayo yataje:-
a.       ______________________________________
b.      ______________________________________
3.      Taja hasara tano (5) za Katiba iliyoandikwa
4.      Taja faida tano (5) za katiba isiyoandikwa
5.      Katika ya Tanzania ni katiba ya kuandikwa au isiyo ya kuandikwa? Eleza kwa nini
6.      Tanzania ni Muungano wa nchi mbili ambazo ni ______________ na ______________
7.      Katiba ya kwanza ya Tanganyika iliandikwa mwaka __________________________
8.      Katiba ya mpito iliundwa kwa sababu zipi? Zitaje
9.      Taasisi gani yenye mamlaka ya kubadili au kurekebisha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uchaguzi wa Kidemokrasia
Uchaguzi ni mchakato ambao huwapa wananchi nafasi kuchagua viongozi ambao watawaongoza kwa muda muda/kipindi fulani. Hivyo uchaguzi utumika kupata viongozi mbalimbali wa taasisi/ofisi kwa mamlaka mbalimbali. Mfano katika jamii, Muungano wa kibiashara, michezo, serikali na nyanja mbalimbali za kiraia na serikali.
Katika nchi ya kidemokrasia watu wanaamini kwamba raia ndio wana haki ya kuchagua kiongozi anayeweza kuwaongoza. Uchaguzi ndio moja kati ya michakato mikubwa katika siasa. Pia uchaguzi ni njia pekee ya kupata amani katika nchi yeyote na kubadilisha madaraka kutoka kwa mtu mmoja/kiongozi mmoja hadi mwingine.
Michakato ya Uchaguzi
Michakato ya uchaguzi hubadilika kutoka nchi moja hadi hadi nyingine, Tanzania ufanya uchaguzi mkuu kila baada ya ya miaka mitano. Pia raia wanaohusika katika uchaguzi huo huanzia miaka 18 na kuendelea ndio wanaohusika. Upigaji wa kura ufanyika kwa siri hivyo kila mtu anatakiwa kuchagua bila woga. Vyombo vya habari vinarusiwa kuwajadili wagombea wa uchaguzi kwa Kuangalia sera za vyama na wagombea wote. Hivyo vyama vya siasa vitachagua wawakilishi wao ili kushiriki katika uchaguzi huo. Mtu anayetaka kugombea nafasi yeyote katika uchaguzi ni lazima ateuliwe kwanza na chama chake cha siasa alichotoka.
Kampeni za Uchaguzi
Kampeni za uchaguzi ni mfulululizo wa Matukio ambayo mgombea na makada wa chama husika hufanya mikutano ya wazi na kunadi sera za vyama vyao kwa nia ya kutafuta wapiga kura kwa mgombea huyo. Hivyo chama kikimchagua mgombea, pia humsaidia kumnadi kwa wananchi wake.
Sifa za Kiongozi Bora katika nchi lazima awe na mambo yafuatayo:-
a.       Mtu anayependa usawa
b.      Awe anaaminika
c.       Awe na maadili na akili timamu
d.      Kuheshimu familia kama kiungo cha jamii
e.       Heshima kwa watu
f.       Kuheshimu haki za binadamu na watu wenye mahitaji maalumu
Uchaguzi wa Wabunge na Rais
Uchaguzi wa rais na wabunge kwa Tanzania unaitwa uchaguzi mkuu. Uchaguzi huo kwa Tanzania hufanyika kila baada ya miaka mitano. Kila chama huteuwa mgombea mmoja kwa kuwakilisha majibo ya uchaguzi kwa nafasi ya wabunge. Katika jimbo kunakuwa na wagombea wengi na kuchaguliwa mmoja katika uchaguzi wa mwisho. Uchaguzi wa wabunge kurudiwa kama mambo yafuatayo yatafanyika:-
                       i.      Kuvunjwa kwa bunge
                     ii.      Mbunge akijiuzuru au kuvuliwa uanachama wa chama chake.
                   iii.      Mbunge akishindwa kutimiza majukumu yake
                   iv.      Mbunge akifa
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
Ni tume iliyoundwa kwa ajili ya kusimamia michakato yote ya uchaguzi katika ngazi zote. Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi uteuliwa na rais na lazima awe jaji kutoka katika Mahakama ya rufaa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kazi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi
                    i.         Kusajili vyama vya siasa
                  ii.         Kusimamia na kuhakikisha sheria na kanuni za uchaguzi zinafuatwa
                iii.         Kupokea malalamiko ya uchaguzi na kutolea maamuzi
                iv.         Kupokea na kugagua mapato na matumizi ya vyama vya siasa
                  v.         Kufuatilia kwa umakini vyanzo vya mapato na matumizi ya ruzuku za serikali kwa vyama vya siasa.
Maswali
1.      Nini maana ya uchaguzi wa Kidemokrasia?
2.      Ni umuhimu wa uchaguzi wa kidemokrasia. Taja faida tano
3.      Ni nani ana haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu Tanzania?
4.      Nini maana kampeni za uchaguzi
5.      Je uchaguzi wa Tanzania Unafanyika kwa kufuata taratibu gani? Zitaje na kufafanua
6.      Taja na eleza kazi saba tu za tume ya taifa ya uchaguzi.
7.      Mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi uteuliwa na nani?


1 comment: